Abstract:
Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa kutathmini matumizi ya tafsiri na mikakati ya
tafsiri katika ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni katika
shule za sekondari nchini Uganda. Utafiti ulikuwa na malengo matatu. Mosi,
kubainisha mikakati ya tafsiri inayotumika. Pili, kutathmini matumizi ya tafsiri na
mikakati ya tafsiri katika ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili na tatu, kubainisha
na kufafanua aina ya changamoto wanazokubana nazo walimu na wanafunzi
wanapotumia tafsiri. Katika mchakato wa kutafsiri, mfasiri hukabiliana na tatizo la
kupata visawe mbadala baina ya lugha chanzi na lugha lengwa. Ili kukabiliana na
tatizo hili, mfasiri hutumia mikakati ya tafsiri. Matumizi ya tafsiri na mikakati ya
tafsiri yanaweza kuwa na athari zake katika uhawilishaji wa ujumbe. Mada
inayoangaziwa katika utafiti huu inahusu uchangamani wa taaluma mbili ambazo ni
tafsiri na ufundishaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni. Kwa hivyo, nadharia moja
isingeweza kutosheleza mahitaji ya uchanganuzi wa data zilizokusanywa. Utafiti
umeongozwa na Modeli ya Vinay na Darbelnet (2004), Nadharia ya Usawe wa
Kidhima ya Nida na Taber (2004) na Nadharia ya Umotishaji Lugha ya Dörnyei
(1994). Utafiti huu ulichukua mkabala mseto. Mbinu zilizotumiwa kukusanyia data
ni pamoja na ushuhudiaji, uchambuzi wa nyaraka na hojaji. Data za utafiti
zimewasilishwa kitaamuli na kitakwimu na kwa kutumia majedwali, chati-duara,
grafumhimili na michoro. Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kwamba walimu na
wanafunzi hutumia tafsiri na mikakati ya tafsiri kwa kiwango kikubwa katika
ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili. Pia, matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba
walimu hutumia mikakati ya tafsiri ili kukabiliana na tatizo la kutafsiri vipashio vya
lugha. Mkakati unaotumiwa mara nyingi katika ufundishaji na ujifunzaji wa
Kiswahili ni tafsiri sisisi, ubadilishaji mtazamo, Ubadilishaji kategoria, Usawe na
tafsiri-mkopo mtawalia. Pia, imebainika kwamba tafsiri inafaa katika ufundishaji na
ujifunzaji wa Kiswahili inapotumiwa pamoja na mbinu nyingine. Kwa kuhitimisha,
matokeo yanaonesha kwamba tafsiri inayotumiwa katika ufundishaji na ujifunzaji wa
Kiswahili ni ya kimawasiliano ambayo ni tofauti na tafsiri-sarufi iliyotumiwa katika
ufundishaji wa Kiyunani na Kilatini. Aidha, matumizi ya tafsiri yana changamoto
zake katika ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili. Inapendekezwa kuratibu mtaala
wa ufundishaji wa Kiswahili ili kuwaongoza walimu wa Kiswahili kutumia
mikabala mseto ambayo pia itajumuisha tafsiri, badala ya kusisitiza mkabala wa
kimawasiliano tu.