dc.description.abstract |
Tasnifu hii inajadili swala la wahusika katika hadithi fupi ya Kiswahili. Tumetumia diwani tatu za hadithi fupi: Kicheko cha Ushindi (1978), Pendo la Heba na Hadithi Nyingine (1996), na Mayai Waziri wa Maradhi na Hadithi Nyingine (2004).
Malengo ya tasnifu hii yalikuwa ni kuchunguza sifa za wahusika wa hadithi fupi, kuonyesha na kuelezea mbinu za usawiri wa wahusika katika hadithi fupi na kukadiria ni kwa kiasi gani mbinu hizi zinavyoweza kuwasawiri wahusika katika ukamilifu wao. Utafti huu umedhihirisha kuwa wahusika katika hadithi fupi ya Kiswahili huwa wakamilifu na watoshelevu kinyume na madai ya wahakiki wengi wa hapo awali. Mtazamo wetu katika utafiti huu ni kwamba mhusika mkamilifu ni yule anayeingiliana vilivyo na vipengele vingine vya hadithi. Pia, waandishi wa hadithi fupi hutumia mbinu mbalimbali ili kuwapa wahusika wao sifa pana na zinazoonyesha utoshelevu wa aina yake.
Tasnifu hii imegawanywa katika sura tano. Sura ya kwanza ambayo ni utangulizi imeshughulikia swala la utafiti, sababu za kuchagua mada, malengo ya utafiti, misingi ya nadharia, yaliyoandikwa kuhusu mada hii na mbinu za utafiti.
Katika sura ya pili tumejadili historia na maendeleo ya hadithi fupi hadi sasa. Sura hii pia imeshughulikia fasiri mbalimbali zinazotolewa kuihusu dhana ya hadithi fupi na
imehitimisha kwa kuangalia sifa bainifu za utanzu huu ambayo zinaupambanua na tanzu nyingine za fasihi ya kiswahili kama vile riwaya, tamthilia na ushairi.
Sura ya tatu imejikita katika kuchunguza mbinu mbalimbali zinazotumiwa kuwaumba na kuwasawiri wahusika wa hadithi fupi. Mbinu hizi ziliweza kujadiliwa moja baada ya nyingine huku zikionyesha jinsi zinavyodhihirika katika hadithi fupi teule. Mihimili ya nadharia mbalimbali zinazozungumzia suala la uhusika na wahusika wa fasihi ilitumiwa katika uchambuzi ili kuwezesha mtafiti kufikia lengo lake.
Sura ya nne imechunguza jinsi wahusika wa hadithi fupi wanavyoingiliana na vipengele vingine vya hadithi kama vile, maudhui, mtindo, ploti, mandhari na kadhalika. Msimamo wa utafiti huu ni kuwa, kutoingiliana vizuri kwa wahusika na vipengele hivi vya hadithi ni upungufu tunaoweza kuelekeza katika uumbaji na usawiri wa wahusika. Iwapo wahusika wataingiliana vizuri na vipengele hivi, majukumu yao katika hadithi yatakuwa wazi na hivyo watakuwa wametekeleza kazi yao ipasavyo. Wahusika wa aina hii basi ni wakamilifu na watoshelevu.
Katika sura ya tano ambayo ni hitimisho, tumetoa muhtasari wa kiini cha tasnifu kwa kugusia maswala yaliyoshughulikiwa katika kila sura kisha tukatoa hitimisho pamoja na mapendekezo ya utafiti wa baadaye. |
en_US |