Abstract:
Mada ya utafiti huu ni kuchunguza uhalisia wa maudhui ya usalama katika fasihi ya watoto mfano wa riwaya ya Kijana Mpelelezi (Wamitila, K.W.2007) na Usiku wa Manane (Kobia, J 2010). Hadithi hizi za watoto zimejikita katika fasihi ya watoto. Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa ni kutathmini uhalisia wa maudhui yanayohusu usalama na yanayonuiwa watoto kama hadhira lengwa, kubainisha maudhui ya usalama yaliyodhihirishwa na waandishi na kueleza jinsi wahusika watoto wanaohusishwa na maudhui ya usalama wanavyosawiriwa na waandishi wa riwaya teule. Nadharia za Uhalisia wa kijamaa na Soshiolojia ya fasihi zilizotumiwa katika utafiti huu zilitoa msingi madhubuti kuwa maswala ya usalama yanayobainika yanafungamana na hali ilivyo katika maisha ya jamii ya karne hii ya ishirini na moja. Vita vya kikabila na ukosefu wa usalama katika jamii yapaswa kuondolewa na kusahaulika kabisa. Hadithi za watoto za waandishi hawa ziliteuliwa kimakusudi kwa kutumia sampuli lengwa kutokana na upekee wa kimaudhui uliodhihirisha uhalisia. Hadithi zilizoteuliwa zilisomwa, data kuhusu uhalisia wa maudhui ya usalama kwa mujibu wa maswali ya utafiti zilioneshwa. Data iliyopatikana kuhusu maudhui ya usalama katika kila hadithi ilichanganuliwa. Mwisho, matokeo na mapendekezo ya utafiti yaliwasilishwa kimaelezo. Matokeo yalionesha kuwa siasa za kikabila zinazoenezwa katika nchi hii kipindi baada ya kipindi, vitisho vinavyoleta migogoro katika jamii na maudhui mengine mengi yanayosabababisha ukosefu wa usalama ni hatari kwa vizazi na vizazi na kuna haja ya kuchukua hatua za dharura kuwafahamisha watoto kupitia hata maandishi kuhusu umuhimu wa amani katika taifa ili wakikua wawe na uwezo wa kueneza maridhiano baina ya makabila yote. Utafiti huu unatarajiwa kuwa muhimu kwa wasomi na waandishi wa fasihi ya watoto. Utafiti huu unaongeza maarifa katika uhakiki wa hadithi za watoto kwa kuangazia mielekeo ya uhalisia wa kimaudhui ya usalama katika jamii. Mwishowe, tumetoa pendekezo la utafiti zaidi.