dc.description.abstract |
Azima ya tasnifu hii ni kufanya uchanganuzi wa kiufafanuzi kuhusu usilimisho wa
maneno mkopo katika LAKĨMŨ kwa kutumia msingi wa kinadharia
uliochangamano. Kila lugha ni tokeo la mabadiliko, hakuna lugha iliyo ya jinsi
moja. Kwa hiyo maneno mkopo huchangia pakubwa mabadiliko haya ya lugha.
Kiswahili ni lugha ya Afrika Mashariki na kati ambayo imekua na kujulikana na
wengi zaidi kuliko lugha nyingine ya Afrika. Vile vile Kiswahili ni lugha ya Kitaifa,
Kibiashara na ya ki+mawasiliano nchini Kenya. Lugha hii imeingiliana na lugha
zingine kwa karne nyingi hali ambayo imesababisha Kiswahili kuwa na utajiri wa
msamiati kuliko lugha zingine za Kibantu.
Tumeibawibu kazi hii katika sura tano. Sura ya kwanza inatoa maelezo ya
kimsingi kuhusu ukopaji wa maneno pamoja na usuli wa utafiti. Mambo
yanayojadiliwa katika usuli huo wa utafiti ni: mada ya utafiti, lugha na jamii
zinazoshughulikiwa, madhumuni ya utafiti, upeo na mipaka ya tasnifu na
udurusu wa maandishi. Pia katika sura hii, tumefafanua sababu zetu za
kuichagua mada hii, msingi wa kinadharia uliotuongoza na vile vile njia za
kufanyia utafiti.
Sura ya pili imeshughulikia ulinganishi wa kifonolojia na kimofolojia wa lugha tatu
zinazomulikwa katika mtalaa huu. Mambo muhimu katika sura hii yanahusu vibadala vya konsonanti na vile vile miundo ya silabi katika usilimisho wa maneno
ya mkopo.
Katika sura ya tatu, tumezijadili sababu za kiisimu jamii zilizochangia ukopaji wa
maneno katika LAKĨMŨ. Sura hii inaipa kazi hii haiba na kuitofautisha na kazi za
awali zilizochunguza maneno ya mkopo. Kwenye sura ya nne, uchanganuzi wa
usilimisho wa maneno ya mkopo umefafanuliwa. Tumebambanua sheria
zinazowakilisha mabadiliko ya kifonolojia katika usilimisho wa maneno mkopo.
Sura ya tano inahitimisha utafiti wetu. Kwenye sura hii, tumetoa muhtasari wa
sura zote pamoja na kujadili kauli muhimu zilizozuka wakati wa utafiti. Fauka ya
hayo tumefasili umuhimu wa tasnifu na kutoa mapendekezo kuhusu vipengele
vya kufanyiwa utafiti. |
en_US |