Abstract:
Imebainika kuwa filamu za Kiswahili nchini Tanzania ni “pacha” wa filamu za ki-Nigeria. Hivyo, makala hii ambayo data zake zilipatakana kwa kutipia na kuchanganua nyaraka imechunguza sababu zinazowasukuma watayarishaji wa filamu za Kiswahili nchini Tanzania kutumia U-Nigeria katika filamu zao. Isitoshe, kwa muhtasari, makala yamegusia utayarishaji wa filamu za Kiswahili nchini Tanzania kama utamaduni mpya wa vijana wenye harakati za kutafuta nafasi yao kijamii pamoja na kujiongezea kipato. Katika makala, dhana ya U-Nigeria imefafanuliwa kama vijenzi mahususi vya hadithi za filamu za ki-Nigeria vinavyorejelea utamaduni na maisha yao ya kila siku. Aidha, vijenzi hivyo vimebainika kujipambanua katika filamu za ki-Tanzania (Kasiga, 2013; Kasiga, 2018). Zaidi ya hayo, makala imebainisha kuwa, sababu kuu ya kutumika kwa U-Nigeria katika filamu za Kiswahili ni utafutaji wa soko la ndani - Tanzania. Sababu nyingine zilizobainishwa zimehusisha ukosefu wa ubunifu, ukosefu wa nyezo bora za utayarishaji wa filamu, ukosefu wa taaluma ya utayarishaji filamu kwa wasanii, na bajeti hafifu za utayarishaji wa filamu za Kiswahili. Hatimaye, makala imependekeza wasanii wa filamu za Kiswahili ni budi kurudi katika misingi ya fasihi ya Kiswahili kwa kuzichukua kazi mfano za fasihi ya Kiswahili na kuzifanya kuwa filamu. Imebainika kuwa kufanyika kwa jambo hilo kutakuwa ni mwanzo bora wa kuhuisha upya utamaduni wa ki-Tanzania kupitia teknolojia ya filamu.