Abstract:
Miiko ni sehemu muhimu inayotoa mwelekeo wa mienendo inayokubalika katika jamii yoyote ulimwenguni. Makala haya yanajadili usawiri wa miiko ya jadi katika jamii ya sasa na mifano ikiwa ni kutoka kwa Wapare wa Mwanga Mkoani Kilimanjaro. Lengo kuu la makala haya ni kubainisha namna miiko ya jadi inavyohusiana na kuakisi moja kwa moja maisha ya jamii katika vipengele nuwai vya maisha. Mjadala wa makala haya uliongozwa na swali lililouliza: Miiko kama kipera kimojawapo cha sanaajadiiya inasawiri vipi maisha ya kila siku ya jamii? Mkabala uliotumika kwenye makala haya ni wa kimaelezo. Mbinu zilizotumika katika utafiti wa makala haya ni mbili. Mbinu ya kwanza ni ya usaili ambayo iliwezesha upatikanaji wa data za awali (msingi) na mbinu ya pili ni ya uchanganuzi wa matini ambayo iliwezesha upatikanaji wa data za upili. Nadharia ya Taalimu Ina Kwao na Fasihi Ina Kwao, ndiyo iliyotumiwa kwenye mwendelezo wa uchunguzi na uchambuzi wa makala haya. Matokeo ya tafiti yalionesha kuwa, miiko ya jadi ni kipera muhimu cha sanaajadiiya kilichofumbata tamathali za semi na hurithishwa kwa njia ya masimulizi. Miiko inasawiri maisha ya jamii na ni mhimili muhimu wa maadili. Miiko hiyo huakisi jamii kitamaduni na kimazingira na hivyo kuendelea kudhihirisha umuhimu usio na shaka.