Abstract:
Tunapokaribia karne moja ya usanifishaji wa Kiswahili, ni dhahiri kuwa ni wachache wanaoongea Kiswahili Sanifu katika mataifa ya Afrika Mashariki na Kati. Hili linatokana na kuwa idadi kubwa ya wakazi wa ukanda huu hujifunza Kiswahili kama lugha ya ziada, huku uhawilisho wa vipengele vya lugha mzazi ukisababisha kuwepo kwa lafudhi mbalimbali. Unyanyapaa wa Viswahili vyenye lafudhi huwapa wasemaji wengi au wazungumzaji watarajiwa kujitilia shaka wanapozungumza Kiswahili. Makala hii inaangazia wahaka wa kiisimu unaowafanya wakazi wa baadhi ya mataifa ya Afrika Mashariki kuambaa kuongea Kiswahili au kupendelea Kiswahili chenye utosarufi. Inapigia debe rajamu pana ya Kiswahili itakayosherehekea tofauti za wazungumzaji katika kupanua matumizi ya Kiswahili. Vilevile inasisitiza kupanuliwa kwa mikabala ya taaluma ya elimulahaja ya Kiswahili ili ijumuishe Viswahili vya kimaeneo vinavyoakisi uhalisia wa sehemu zote kinakozungumzwa. Makala hii inahitimisha kwa kutoa wito wa kufanya utafiti zaidi kuhusu wahaka wa kiisimu ili kuondoa ubaguzi wa kiisimu unaotokana na unyanyapaa. Hili ndilo litakalofanya rajamu ya Kiswahili imilikiwe na ikubalike na watu wote wanaozungumza Kiswahili.