Abstract:
Makala hii inajadili ontolojia ya nafsi katika riwaya teule za Muhammed Said Abdulla kwa kujiegemeza katika kipengele cha kani. Kimsingi, kila mwanadamu ana nafsi. Nafsi ni kipengele kinachotazamwa kama uhai, roho pamoja na moyo (Kaponda, 2018). TUKI (1981) wanafasili dhana ya nafsi kuwa ndiyo roho au kiini cha dhati ya jambo husika. Hivyo, nafsi huongoza hali ya kupumua na kuupa uhai mwili wa mwanadamu. Aidha, kila nafsi inaongozwa na kani ambayo aghalabu huwa ni fiche. Data za msingi zilizofafanuliwa katika makala hii zimepatikana maktabani na uwandani kwa kutumia mbinu ya usaili na uchambuzi wa maandiko. Nadharia ya Nje- Ndani ilitumika katika kuongoza mjadala. Matokeo ya mjadala yanaonesha kuwa nafsi kiontolojia haiwezi kuonekana lakini kani yake inabainika katika matendo, lawama, kupaparika, kutulia na kuamrisha maovu. Ithibati ya matokeo haya yametolewa kutoka katika riwaya tatu za Muhammed Said Abdulla ambazo ni Duniani Kuna Watu, Kosa la Bwana Msa, na Kisima cha Giningi.