Abstract:
Lugha ya Kiswahili imekuwa bidhaa adimu kwa miaka ya hivi karibuni kutokana na fursa za ajira zinazopatikana ndani yake (Mahenge, 2021). Miongoni mwa fursa hizo ni tafsiri, ukalimani, ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni, ufundishaji wa Kiswahili nje ya nchi na uandishi na uchapishaji wa nyaraka za Kiswahili. Wadau mbambali nchini Tanzania wamechangamkia fursa hizo ili kunufaika kiuchumi. Hata hivyo, zipo changamoto zinazojitokeza katika kunufaika na fursa zilizopo katika lugha ya Kiswahili nchini Tanzania. Kwa hiyo, lengo la makala hii ni kuchunguza changamoto katika ubidhaishaji wa Kiswahili na kupendekeza njia za kutatua changamoto hizo. Data za makala hii zimekusanywa Jijini Mwanza katika kongamano la wadau wa Kiswahili. Watoa taarifa 36 walihusika katika kutoa data za utafiti huu. Watoa taarifa hao waliteuliwa kwa kutumia usampulishaji lengwa. Mbinu zilizotumika katika ukusanyaji wa data ni hojaji na usaili. Aidha, uwasilishaji wa data ulitumia mbinu ya maelezo. Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa ubidhaishaji wa lugha ya Kiswahili nchini Tanzania hukumbwa na ubeberu wa lugha za kigeni katika Kiswahili, dhana potofu kuhusu lugha ya Kiswahili, utamaduni hafifu wa kujisomea, kukosekana kwa taarifa sahihi kuhusu ajira nje ya nchi, uhusikaji wa wasiowataalumu katik shughuli za taaluma za Kiswahili na ufinyu wa soko la ajira nje na ndani ya nchi. Vilevle, makala imebainisha kuwa, mbinu za utatuzi wa changamoto hizo ni uimarishaji wa mafunzo kwa walimu wa Kiswahili kwa wageni, BAKITA kutoa leseni kwa taasisi au watu wanaojishughulisha na taaluma za Kiswahili kama vile wafasiri, wakalimani na watoamafunzo ya Kiswahili kwa wageni.