Abstract:
Ufundishaji wa Kiswahili katika shule za sekondari nchini Uganda unachukua
mwelekeo wa ufundishaji wa lugha ya kigeni kwa sababu wajifunzaji hawapati
ingizo kutoka katika jamii. Lengo la makala hii ni kuchunguza tafsiri kama
nyenzo ya ufundishaji wa lugha ya kigeni nchini Uganda. Madhumuni yake ni
kuonesha kwamba ingawa tafsiri hupingwa na baadhi ya wataalamu katika
ufundishaji wa lugha ya kigeni, ina nafasi yake na haiwezi kuepukika katika
miktadha maalumu kama ilivyo nchini humo. Makala inaibua hoja kwamba
tafsiri inayotumika katika ufundishaji wa Kiswahili ni ya kimawasiliano
ambayo ni tofauti na tafsiri-sarufi inayojiegemeza kutafsiri kaida za lugha. Ili
kufikia lengo la makala hii, data ilikusanywa kwa njia ya hojaji kutoka kwa
wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha pili waliokuwa wakisoma Kiswahili
katika shule za sekondari jijini Kampala. Wengi wa wanafunzi hao walianza
kusoma Kiswahili kuanzia kidato cha kwanza, yaani hawakusoma Kiswahili
shule ya msingi. Nadharia ya Umotishaji Lugha ilitumika kuchanganua data za
makala hii ambayo imezingatia maboresho yaliyofanywa na Dörnyei (1994).
Matokeo yanaonesha kwamba tafsiri ya kimawasiliano hutumika katika
ufundishaji wa Kiswahili nchini Uganda katika shule za sekondari. Aidha,
matokeo yanaonesha kuwa tafsiri hutumika kama nyenzo ya ufundishaji kwa
lengo la kuwapa motisha wajifunzaji katika mazingira ambayo hawapati ingizo
kutoka kwa jamii.