Abstract:
Tamthilia ya Kiswahili ina historia fupi ikilinganishwa na tanzu zingine, hasa ushairi. Tamthilia za kwanza kuwahi kutafsiriwa kwa Kiswahili na zilizoandikwa kwa lugha hii zilizingatia sana maudhui ya kidini, kizalendo, utetezi dhidi ya dhuluma za tawala za kigeni na hasa ukoloni mamboleo. Kinyume na hali hiyo, tamthilia ya Kiswahili katika kipindi cha kuanzia 1950 hadi miaka ya 2020 imesheheni wingi wa tungo zinazosifia Uafrika na heshima ya mtu mweusi hapa barani Afrika na kote ulimwenguni. Uchunguzi wa tamthilia hizi unadhihirisha kujitolea kwa dhati kwa watunzi wake kuelezea, kutetea na kuhimiza heshima ya Mwafrika. Maudhui yake yanakiuka yale masuala mapevu ya utaifa, uraia na tawala za mataifa ya Kiafrika. Kwa sababu hii, makala hii imenuia kuchunguza namna suala la heshima na kujitambua kwa Mwafrika limeshughulikiwa katika tamthilia ya kisasa. Ili kufikia lengo hili, makala imechunguza kwa kina namna suala hili limesawiriwa katika tamthilia ya Mashetani Wamerudi (Mohamed 2016). Tamthilia hii iliteuliwa kwa kutumia mbinu kusudio. Hii ni kwa sababu usomi awali ulionyesha kuwa tamthilia hii imetumia misingi ya nadharia ya Ujumi Mweusi. Data yenyewe ilikuwa ya kitaamuli na ilichanganuliwa vilevile kwa njia ya kinathari. Makala yalionyesha namna ambavyo mwandishi ameweka wazi hadhi ya Mwafrika na kudhihirisha kuwa amejitambua na anapaswa kutambuliwa na kuheshimiwa na ulimwengu mzima. Hii ni baada ya Mwafrika kuelewa kwamba watu kutoka mabara mengine sio bora kuliko yeye kama ambavyo watu hawa hutaka ieleweke na Mwafrika.