Abstract:
Makala hii inafafanua ujumi unavyoakisi hali halisi ya jamii katika hurafa za Wapemba. King’ei (2019), akizungumzia kuhusu Ujumi mweusi, ameeleza kuwa ni tangamano la itikadi, falsafa na maoni ambayo yalikusudiwa kutetea hadhi ama utu, uhuru na utamaduni wa Mwafrika. Amesisitiza pia kuwa falsafa hii ilinuiwa kuwa jibu dhidi ya udunishwaji wa Mwafrika katika historia, elimu, dini na falsafa ya Kimagharibi. Kwa kuwa nadharia ya ujumi wa Mwafrika katika kueleza uzuri wa kiidili husisitiza kuwa hakuna uzuri mmoja kwa jamii zote, kila jamii huwa na namna yake na ya kipekee katika kuuthamanisha ujumi kwenye mazingira na nyakati zilizopita. Mhakiki bora wa uzuri wa kiujumi kwa misingi ya idili, anapaswa kuwa ni zao la jamii hiyo au mtu aliyejifunza utamaduni wa jamii hiyo kwa muda mrefu. Pia, kama asemavyo Sanga (2019, uk. 26), vigezo vya kiujumi vya kiidili ni fiche, navyo hutupasa kurejelea kwenye muktadha wa utamaduni wa jamii husika. Kwa njia ya upitiaji na uchambuzi wa nyaraka, makala hii inaonesha ujumi unavyoweza kuiakisi hali halisi ya jamii kupitia hurafa za Wapemba. Tumefafanua kwamba ujumi unaweza kuiakisi hali halisi ya maisha, kupitia vipengele vya kiutamaduni, sanaa jadi/ya za Kiafrika, masimulizi na maudhui ya Kiafrika pamoja na mandhari.