Abstract:
Makala hii inachanganua mbinu zinazotumika katika kufundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni ili kuwezesha uzingativu wa utamaduni jamii. Tafiti mbalimbali zimeonesha mchango wa mbinu za kufundishia lugha kwa wajifunzaji Kiswahili kama lugha ya kigeni. Licha ya kuwepo uhusiano kati ya utamaduni jamii na ufundishaji wa lugha darasani, tafiti hazijaonesha namna mbinu hizo zinavyoweza kutumika ili kuwezesha uzingativu wa utamaduni jamii. Utafiti huu umezingatia mkabala wa kitaamuli. Data zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya usaili huria kwa walimu, na kuchambuliwa kwa kutumia mbinu ya kusimba maudhui. Vituo na taasisi za MS Training Centre for Development Cooperation, Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, na Kiswahili na Utamaduni ndizo zimehusishwa. Nadharia ya Umahiri wa Kimawasiliano na Tamaduni Mchanganyiko ya Hall (1992) imetumika katika makala hii. Matokeo yamedhihirisha mbinu zifuatazo hutumika miongoni mwa wafundishaji wa Kiswahili: Matumizi ya teknolojia, mbinu ya uzamaji kindakindaki, mbinu ya maelezo au ufafanuzi, mbinu ya ufaraguzi na mbinu ya vitendo halisi. Kwa hivyo, makala hii inapendekeza kuwa ni muhimu sana katika taasisi na vituo husika kuwa na programu za kuwaelekeza walimu namna bora ya kutumia mbinu hizi ili kuzingatia utamaduni jamii. Vilevile, tafiti mbalimbali zifanyike kuonesha changamoto zinazowakabili walimu katika uzingatiaji wa utamaduni jamii darasani.