dc.description.abstract |
Makala hii inahusu uhakiki wa usawiri wa taashira ya uongozi katika nchi za Afrika, hasa zile zilizowahi kutawaliwa na mbeberu, kwa kujikita katika tamthilia ya Kiswahili. Tamthilia iliyohakikiwa ni moja ambayo imeandikwa na Kimani Njogu: Zilizala. Nia ya uhakiki huu ilikuwa kujadili namna mwandishi huyu ameusawiri uongozi barani Afrika kitaashira kwa lengo la kuukosoa na kuuelekeza. Makala hii iliongozwa na Nadharia ya Baada ya Ukoloni. Nguzo zilizoongoza uchanganuzi wa data ya makala hii ni pamoja na vita vya uhuru, ukoloni mamboleo, na uzinduzi mintarafu ya kusudi la uhakiki wa makala. Zilizala ilichaguliwa kimakusudi kutokana na maudhui makuu ya uongozi yanayojadiliwa na mwandishi. Kimani Njogu alifanikiwa kulisawiri suala la uongozi katika mataifa mengi barani Afrika, hususani Kenya kwa kutumia kazi ya kifasihi ili kuepuka kukaripiwa na utawala au hata uongozi wowote ule. Suala kuu lililodhihirika katika tamthilia hii ni la ukoloni mamboleo kupitia istilahi ya kitafsida ya utandawazi. Kupitia mhusika Udenda, mwandishi alifanikiwa kutumia mbinu ya taashira kuusawiri uongozi katika nchi za Afrika paruwanja, ingawa kwa njia kwepi na fiche. Mhusika huyu na wengine kadhaa wametumiwa na mwandishi wa tamthilia hii kuwasawiri viongozi wengi barani Afrika, kitaashira, kama vikaragosi vya viongozi wa mataifa ya Japani, Urusi, Uropa na Marekani. Makala hii imedhihirisha baadhi ya mbinu wanazotumia viongozi wa mataifa kwasi na vikaragosi vyao kujinufaisha wao wenyewe huku wananchi katika mataifa tofautitofauti barani Afrika yenye uwezo wa kujiendeleza na kujitegemea wakiendelea kupapatika kwa kusombwa na mawimbi katika bahari la ulofa, ndwele, njaa, na ukame wa kila aina, na hatimaye wanaangamia. |
en_US |