Abstract:
Lugha ya Kiswahili kama zilivyo lugha zingine ina kawaida ya kutohoa maneno kutoka lugha mbalimbali. Miongoni mwa maneno yanayotoholewa ni maneno changamani, yaani neno moja linaloundwa na maneno zaidi ya moja; mfano, neno Bongofleva (lililotokana na kirai cha Kiingereza Bongo Flavour). Kumekuwa na mkanganyiko wa mawazo kuhusu maana ya Bongofleva na mwasisi wa neno hilo. Makala hii inaonesha mawazo mbalimbali yanayokinzana kuhusu masuala hayo mawili. Makala hii ni matokeo ya mapitio ya maandiko na tajiriba ya mwandishi katika uga wa muziki wa Bongofleva akiwa mdau, mfuatilitiaji, mchambuzi na msanii wa muziki huo. Aidha, sehemu ya data zilishadidiwa kwa kufanya mahojiano na msanii na mtangazaji wa zamani aitwaye KCB. Makala hii imebaini kwamba jina “Bongofleva” liliasisiwa na kutumiwa kwa mara ya kwanza na Mhagama Pesambili (aliyewahi kuwa mtangazaji wa Radio One) na KCB katika kipindi cha DJ Show. Kuhusu maana ya Bongofleva, makala inapendekeza kwamba aina zote za miziki zinazopatikana nchini Tanzania zipo chini ya mwamvuli (kapu) wa Bongofleva kwa kujikita katika mantiki kwamba Bongofleva ni neno lililotoholewa kutoka katika lugha ya Kiingereza “Bongo Flavour” likiwa na maana ya msingi ambayo ni ladha kutoka Bongo/Dar/Tanzania.