Abstract:
Makala hii imechunguza athari za matamshi ya lugha za jamii zinavyosababisha ukiushi wa maana katika maneno ya Kiswahili Sanifu. Hoja kuu katika makala hii ni kuwa, pamoja na kuwapo kwa tafiti anuwai zilizodhihirisha vipengele mbalimbali vya matamshi vilivyotokana na kuathiriana kati ya lugha za jamii na Kiswahili, bado kwa kadri ya uelewa wetu hakuna tafiti zilizobainisha athari za ukiushi wa maana za maneno zinazotokana na kuathiriana kati ya lugha hizo. Data za msingi katika makala hii zimekusanywa maktabani na uwandani kwa kutumia mbinu za usomaji makini na mahojiano. Matokeo ya uchunguzi yanaonesha kwamba kuna vipengele mbalimbali vya matamshi katika lugha za jamii vinavyoathiri maana katika matumizi ya Kiswahili Sanifu. Mathalan, matumizi ya sauti [f] badala ya [v], [a] badala ya [h], [bh] badala ya [b] na [l] badala ya [r] na kinyume chake. Athari za matumizi ya sauti hizo ni kubadilisha matamshi, udondoshaji na kuathiri maana za maneno, katika Kiswahili Sanifu. Pia huchangia kuibuka kwa maneno ambayo hayafahamiki kabisa katika Kiswahili Sanifu. Makala hii inatoa mchango kwa watumiaji wa Kiswahili wageni na hata wenyeji wanaojifunza lugha ya Kiswahili kufahamu Kiswahili Sanifu na maana za maneno kwa usahihi wake. Hivyo, ni muhimu kuzingatia matamshi sahihi ya maneno ya Kiswahili Sanifu kwani matamshi yana mfungamano mkubwa na maana za maneno. Kutokana na hali hiyo, ndio maana kubadili sauti katika matamshi ya maneno kunabadili pia maana halisi za maneno yaliyokusudiwa.