Abstract:
Makala hii imechunguza ujitokezaji wa nomino za Kiswahili zinazoibua maana za kitashibiha katika riwaya ya Zawadi ya Ushindi na Watoto wa Maman’tilie. Data zilipatikana kwa uchanganuzi matini maktabani kwa usomaji makini wa riwaya teule. Matokeo ya utafii yaliyozaa makala hii yameonesha kuwa nomino ni kijenzi muhimu katika muundo wa kuibua maana ya kitashibiha. Pia, yameonesha kuna nomino za wazi na nomino fiche kwenye kazi za kifasihi zinazoibua maana za kitashibiha. Nomino hizi hutumiwa kwa lengo la kuonesha ubunifu na upekee wa kifasihi ambao wasanii hulinganisha hali za maumbile na tabia za jamii ili kutoa mafunzo, kupamba lugha na kuufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa jamii iliyolengwa kupitia tashibiha. Nomino fiche za makala hii zimeibua maana za kitashibiha kupitia nafasi, muundo na matumizi ya nomino kulingana na muktadha wa sentensi za Kiswahili. Makala hii inapendekeza kuwa wataalamu wa fasihi wanapaswa kuchunguza suala la maana za kitashibiha kwenye tanzu zote za fasihi ili kubaini darajia za maneno hasa vitenzi vinavyobeba dhima za kifasihi na kisarufi katika kuibua maana za kitashibiha ili kusaidia dhana ya fasihi linganishi.